EAC yapongeza uchaguzi wa Rwanda kuwa ni wa amani na wenye kuaminika
2024-07-19 09:06:01| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Alhamisi ilisema uchaguzi wa Rwanda uliofanyika Jumatatu ni wa amani, na unaonyesha matakwa ya watu kwa ujumla. Kwenye uchaguzi huo rais wa sasa Paul Kagame amechaguliwa tena kuwa rais.

Ikitoa taarifa mjini Arusha, Tanzania EAC ilisema mchakato wa uchaguzi wa Rwanda ulipangwa vizuri bila ya kuwa na vurugu yoyote, hatua ambayo ni muhimu kwenye mchakato wa mageuzi ya nchi hiyo.

Jaji mkuu wa zamani wa Kenya ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa EAC wa waangalizi wa uchaguzi wa Rwanda, David Maraga alipongeza vyombo vya habari vya umma nchini Rwanda kwa kuripoti habari zenye uwiano na usawa kwa ajili ya wagombea wote wa nafasi ya urais na vyama vyote kabla ya uchaguzi, na kuhimiza mchakato wa uchaguzi wenye amani na uwazi. Aliongeza kuwa Tume ya Uchaguzi ya Rwanda imefanya maandalizi ya kutosha na kudumisha uwazi katika usimamizi wa uchaguzi.