Afrika Kusini yaadhimisha Siku ya Mandela
2024-07-19 09:07:43| CRI

Serikali ya Afrika Kusini na raia wa tabaka mbalimbali, Alhamisi waliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, ambayo pia inajulikana kama Siku ya Mandela, kwa kutoa michango yao chanya katika jamii kote nchini.

Katika taarifa yake serikali ya Afrika Kusini ilisema Siku ya Mandela ya 2024 ina umuhimu wa kipekee kwa sababu, katika siku kama hii mwaka 1994, Rais wa zamani Mandela aliongoza Serikali ya kwanza ya Umoja wa Kitaifa.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa mwaka 2024 ni maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa serikali ya kidemokrasia ya Afrika Kusini, hatua ambayo ni muhimu iliyofikiwa na Mandela, na duniani kote, ambapo amekuwa alama ya uhuru na demokrasia.

Msemaji wa serikali Nomonde Mnukwa alitoa wito kwa watu binafsi, jamii na wafanyabiashara kuunga mkono shirika la hisani au kusaidia watu wasiojiweza, wakiwemo walioathirika na mafuriko na majanga mengine ya asili ambayo yameathiri nchi hivi karibuni, katika siku hii ya Mandela.

Siku ya Mandela, huadhimishwa kila mwaka Julai 18, ambayo ni siku ya kuzaliwa kwake na kauli mbiu ya mwaka huu ni "Uwezo wa kupambana na umaskini na ukosefu wa usawa bado uko mikononi mwetu,".