Polisi wa Kenya wapiga marufuku maandamano katikati mwa jiji la Nairobi
2024-07-19 09:11:59| CRI

Polisi wa Kenya Alhamisi wamepiga marufuku maandamano dhidi ya serikali katika wilaya ya kati ya biashara na viunga vyake huko Nairobi, wakitaja wasiwasi wa usalama.

Zaidi ya watu 50 wameuawa, na wengine makumi kujeruhiwa na mali kuharibiwa tangu maandamano ya kuipinga serikali yalipoanza nchini Kenya mwezi Juni. Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, katika taarifa iliyotolewa Jumatano jioni, alisema mamlaka ilipokea taarifa za kijasusi za kuaminika kwamba vikundi vya uhalifu vilivyopangwa vinapanga kuchukua fursa ya maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali kutekeleza vitendo vya uhalifu.

Alisema kukosekana kwa kiongozi wa wazi miongoni mwa waandamanaji wengi vijana kumefanya kuwa vigumu kwa polisi kutekeleza itifaki za usalama.

Wakati huohuo Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura alisema nchi hiyo imepoteza takriban shilingi bilioni 6 (karibu dola za Kimarekani milioni 45.8) kutokana na maandamano hayo. Amewataka waandamanaji kufikiria upya mipango yao ya kufanya maandamano katika siku zijazo kwani malalamishi yao yameshughulikiwa.

Katika wiki zilizopita Rais William Ruto amechukua hatua kadhaa kali ili kukidhi matakwa ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kutupilia mbali mapendekezo mapya ya ushuru yaliyomo katika Mswada wa Sheria ya Fedha 2024, kuweka hatua za kubana matumizi, na kuvunja baraza lake lote la mawaziri. Mwaura alisema rais ameazimia kuwa na mazungumzo na vijana kama ilivyodhihirishwa na mazungumzo yake pamoja nao hivi karibuni kwenye X, iliyokuwa Twitter.