Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza nia ya kujitoa katika mbio za urais katika uchaguzi ujao nchini humo, ikiwa ni baada ya idadi kubwa ya wabunge wa chama cha Democrat kueleza wasiwasi wao juu ya uwezo wake katika uchaguzi huo.
Katika taarifa iliyotumwa kupitia mtandao wa kijamii wa X, rais Biden amesema ingawa ilikuwa nia yake kugombea tena nafasi ya urais, anaamini kuwa ni kwa maslahi ya chama na taifa kwake kujitoa katika nafasi hiyo na kujikita zaidi katika kutimiza majukumu yake kama rais kwa kipindi kilichobaki.
Katika hatua nyingine, rais Biden amesema anaunga mkono kikamilifu na kumpendekeza Makamu wake Kamala Harris kuwa mgombea wa Chama cha Democrat katika uchaguzi wa mwaka huu.