Rais wa Rwanda avunja rekodi yake kwenye uchaguzi
2024-07-22 14:44:08| cri

Rais Paul Kagame wa Rwanda amevunja rekodi yake binafsi kwenye uchaguzi wa Rwanda, kwa kupata asilimia zaidi ya 99% ya kura kwenye matokeo kamili ya uchaguzi wa nchi hiyo. Ushindi huo ni zaidi ya ule wa uchaguzi wa mwaka 2017 alipopata 98.63% ya kura, na zaidi ya 93% aliyopata mwaka 2010 , na 95% mwaka wa 2003.

Ushindi huo unatajwa kuwa unatokana na umaarufu wake mkubwa, huku Rwanda ikiwa imepata utulivu na ukuaji wa uchumi chini ya utawala wake.

Wagombea wawili kwenye uchaguzi huo, Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana wa kujitegemea walichuana na Rais Kagame, na kupata 0.53% na 0.32% mtawalia. Tume ya uchaguzi ya Rwanda imesema 98% ya watu walijitokeza kupiga kura.

Ushindi wa Bw Kagame umesifiwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, ambaye amesema kuchaguliwa kwake tena ni ushahidi wa imani waliokuwa nayo Wanyarwanda kwa uongozi wake.