Umoja wa Afrika umeanza mkutano wake wa sita wa katikati ya mwaka jumapili iliyopita mjini Accra, Ghana, na kutoa wito wa amani na mshikamano katika bara hilo.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Elimu na Ujuzi wa Afrika kwa Karne ya 21” umewakutanisha watu mbalimbali wakiwemo wajumbe kutoka Umoja wa Afrika na Jamii za Kiuchumi za Kikanda.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesisitiza nafasi ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) katika kuboresha maingiliano katika bara hilo. Pia amezitaka nchi za Afrika kutumia vizuri fursa ya Eneo hilo na kulifanya kuwa injini ya ukuaji na uchumi anuwai ili kuongeza biashara ndani ya bara hilo.
Naye rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo amesema, baadhi ya kanda barani Afrika bado zinakabiliwa na machafuko, ukosefu wa usalama na vurugu zinazozuia maendeleo na kuwa tishio kwa usalama mzima wa kikanda. Amewataka marais wa nchi za Afrika kufanya kazi kwa bidii kupata suluhisho la migogoro mbalimbali katika bara hilo.