China yaisaidia Zimbabwe kuchimba visima kukabiliana na ukame
2024-07-23 08:38:10| CRI

Visima 300 vitachimbwa katika mikoa minne ya Zimbabwe chini ya mradi unaofadhiliwa na China wa kuchimba visima uliozinduliwa jana jumatatu katika mji wa Mahusekwa, mkoa wa Mashonaland Mashariki nchini Zimbabwe.

Mradi huo umetokana na tangazo la hali ya dharura lililotolewa na rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa Machi 3 mwaka huu kutokana na ukame uliosababishwa na hali ya hewa ya El Nino unaoikabili nchi hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nyumba na Masuala ya Kijamii wa Zimbabwe, Danuel Garwe amesema, mradi huo utakuwa na athari chanya kwa maisha ya watu katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya na ukame katika mikoa wa Mashonaland Mashariki, Manicaland, Masvingo na Midlands.

Amesema mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya China ya Geo-Engineering, utakuwa na msaada mkubwa katika kupunguza uhaba wa maji katika mikoa hiyo minne.

Naye Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding amesema, mradi huo ni ushuhuda mwingine wa urafiki thabiti kati ya Zimbabwe na China, na kwamba anatumai kuwa visima hivyo vitasaidia kupunguza makali ya ukame kwa Wazimbabwe.