Watu 600 wameuawa tangu tarehe 10 mwezi Mei katika mapigano yanayoendelea kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Mwitikio wa haraka (RSF) katika mji mkuu wa mkoa wa Darfur Kaskazini, El Fasher.
Mkurugenzi mkuu wa Wizara ya Afya ya Mkoa wa Darfur Kaskazini, Ibrahim Khatir amesema, idadi ya vifo huenda ikaongezeka zaidi kwa sababu baadhi ya waathiriwa wamezikwa na wanafamilia bila ya kufikishwa hospitali. Ameelezea hali katika mji wa El Fasher kuwa na utulivu kiasi, licha ya hospitali nyingi na vituo vya afya kufungwa kutokana na mashambulio ya makombora.
Sudan imekumbwa na mapigano makali kati ya jeshi la nchi hiyo na kikosi cha RSF tangu mwezi April mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu 16,650, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Juni na Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.