Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imesema hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu imerekodi ongezeko la asilimia 13 la abiria waliofika kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2023. TAA pia imesema ina mpango wa kukarabati na kujenga vyumba vipya vya mapumziko vya abira mashuhuri (VIP) katika viwanja vya ndege vya Mwanza na Arusha, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), katika jitihada zake za kuboresha huduma zinazotolewa kwa watalii na wawekezaji wanaofikia Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura amesema abiria waliofika nchini Tanzania kupitia viwanja vya ndege wameongezeka kutoka milioni 2.8 waliorekodiwa mwaka 2023 hadi milioni 3.8. Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 13, na matumaini yake ni kwamba tangu kuanza kwa msimu wa baridi, abiria wanaowasili kupitia Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya JNIA, KIA na Abeid Amani Karume (AAKIA) wataongezeka zaidi.