Wataalamu wanakutana nchini Kenya kujadili njia za kuboresha sekta ya maziwa barani Afrika
2024-07-25 08:42:44| CRI

Watalaamu wameanza mkutano wa siku tatu mjini Nairobi, Kenya, jana jumatano kwa lengo la kujadili njia za kuboresha sekta ya maziwa barani Afrika.

Mkutano wa Ufundi wa Sekta ya Maziwa barani Afrika umekutanisha zaidi ya washiriki 100 na wajumbe 500 wanaojumuisha maofisa kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa, maofisa wa ngazi ya juu wa serikali za nchi za Afrika, na wataalamu wa sekta ya maziwa, na wanabadilishana maoni kuhusu maendeleo ya sasa ya teknolojia katika sekta ya maziwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo nchini Kenya, Jonathan Mueke amesema, nchi hiyo ilizalisha lita bilioni 5.2 za maziwa mwaka jana, ambazo kati yao ni asilimia 40 tu ilitumika baada ya kuongezewa thamani. Takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Takwimu ya Kenya zinaonyesha kuwa, sekta ya maziwa inawasaidia wakulima wadogo milioni 1.8 na kuchangia asilimia 4.5 ya uchumi wa nchi hiyo.

Kaimu mwakilishi wa FAO nchini Kenya, Tipo Nyabenyi amesema, mkutano huo utatoa jukwaa kwa sekta ya maziwa barani Afrika kutambua teknolojia za kisasa zitakazosaidia kupanua sekta ya maziwa barani humo.