China na Russia zimekubaliana kupanua zaidi uwekezaji na ushirikiano kwenye sekta ya nishati ili kukuza uhusiano wa pande mbili.
Ahadi hizo zimetolewa kwenye mkutano wa 11 wa Kamati ya Ushirikiano wa Uwekezaji kati ya China na Russia, ulioongozwa na naibu waziri mkuu wa China Bw. Ding Xuexiang, aliyefanya ziara nchini Russia kuanzia Jumapili hadi Jumanne, na naibu waziri mkuu wa kwanza wa Russia Bw. Denis Manturov, mkutano wa 21 wa Kamati ya Ushirikiano wa Nishati ya China na Russia ulioongozwa na Bw. Ding na naibu waziri mkuu wa Russia Alexander Novak, na Kongamano la 6 la Biashara ya Nishati kati ya China na Russia, ambalo Bw. Ding pia alihudhuria.
Wakati akiongoza mikutano hiyo, Bw. Ding, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, alibainisha kuwa marais wa nchi hizo mbili wamefanya mazungumzo mengi ya kimkakati na kufikia mfululizo wa maafikiano muhimu, na kupanga mpango mpya wa maendeleo ya uhusiano na ushirikiano kati ya China na Russia katika nyanja mbalimbali.
Bw. Ding alisema China inapenda kushirikiana na Russia kutekeleza kwa dhati maafikiano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuendelea kuboresha kiwango cha uwekezaji na ushirikiano wa nishati kati ya nchi hizo mbili, na kuleta manufaa kwa pande zote, matokeo ya kunufaishana na maendeleo ya pamoja.
Ukisifu maendeleo ya uhusiano kati ya Russia na China na mafanikio ya ushirikiano wa kivitendo, upande wa Russia umepongeza kuitishwa kwa Mkutano wa Tatu wa Wajumbe Wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na kusema mageuzi muhimu yaliyotajwa kwenye azimio lililopitishwa katika mkutano huo si tu kwamba yatahimiza ustawi na maendeleo ya China, bali pia yatatoa fursa mpya kwa maendeleo ya uhusiano kati ya Russia na China.