Mahakama ya kijeshi ya DRC yafungua kesi dhidi ya viongozi wa kundi la M23
2024-07-25 08:43:17| CRI

Mahakama ya kijeshi ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefungua mashtaka dhidi ya Corneille Nangaa, kiongozi wa kisiasa wa kundi la Muungano wa Mto Kongo (AFC) lenye uhusiano na kundi la waasi la M23.

Nangaa ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi ya DRC na watu wengine 25 wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita, kushirikiana na makundi ya uhalifu, na uhaini.

Wengine waliofunguliwa mashtaka ni pamoja na kiongozi wa kundi la M23 Sultani Makenga, kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo Betrand Bisimwa, na wasemaji wa kundi hilo Willy Ngoma na Lawrence Kanyuka.

Hali ya wasiwasi na mgogoro wa kibinadamu umelikumba eneo la mashariki mwa DRC licha ya kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano hadi Agosti 3 kati ya jeshi la DRC na waasi wa kundi la M23 ambao wanashikilia vijiji 100 katika sehemu ya mashariki mwa mkoa wa Kivu Kaskazini.