Kampuni inayotoa huduma za mtandao nchini Zimbabwe Dandemutande jana imezindua rasmi makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya mawasiliano ya simu ya China China Telecom ili kutoa huduma ya kasi ya mtandao kwa wafanyabiashara wa China nchini humo.
Ofisa mkuu mwandamizi wa kampuni hiyo Never Ncube amesema, ushirikiano huo unawezesha wafanyabiashara wa China nchini Zimbabwe kupata huduma ya kasi na ya kuaminika ya mtandao kutoka Zimbabwe hadi China. Amesema ushirikiano wa kampuni hiyo na kampuni ya China Telecom unahakikisha kuwa kuna njia maalum iliyotengwa hususan kwa wafanyabiashara wa China, na hivyo kupunguza ucheleweshaji wa shughuli za kibiashara.
Meneja mkuu wa kampuni ya China Telecom nchini Afrika Kusini Zhang Guangzhu amesema, kampuni hiyo daima imejikita katika kuboresha maingiliano barani Afrika.