Tanzania imefanya majaribio ya safari ya treni ya reli ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma, ambapo zaidi ya watu 900 walifurahia safari hiyo bila malipo kutoka pande zote mbili.
Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa, safari hiyo yenye umbali wa kilomita 541 ilichukua muda wa saa tatu na dakika 25.
Kadogosa amesema treni iliyotumiwa kwa ajili ya majaribio hayo ina mabehewa 14 na iliondoka Dar es Salaam saa 12:00 asubuhi kwa saa za huko, na kuwasili Dodoma saa 3:25 asubuhi.
Kadogosa ameongeza kuwa huduma ya reli ya SGR inawakilisha maendeleo makubwa katika miundombinu ya nchi hiyo, na itaongeza ufanisi na uunganishaji, na kwamba uzinduzi wa reli hiyo unatarajiwa kuleta mapinduzi ya usafiri nchini Tanzania kwa kupunguza muda wa safari na kukuza shughuli za kiuchumi nchini humo.