Mbaroni kwa kumpa mimba mtoto wake
2024-07-29 23:16:22| cri

Mahakama ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe imemfikisha mahakamani Issa Mgode (44), mkazi wa Kijiji cha Kokoto, Kata ya Mpemba, Wilaya ya Momba kujibu shtaka la kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake wa kufikia (13) jina limehifadhiwa.

Mkuu wa Mashtaka Wilaya ya Momba, Simon Peres alisema mshtakiwa aligundulika kufanya kosa hilo Juni 29, mwaka huu baada ya mtoto wake wa kufikia aliyekuwa akimlea kutokana na kumuoa mama yake kugundulika ana ujauzito baada ya kupimwa afya na mama yake aliyefanya uamuzi huo baada ya mabadiliko ya kimwili kwa mtoto huyo.

Peres alisema mtoto huyo aliieleza mahakama kuwa baba yake wa kambo alianza kumbaka tangu Aprili, 2024 baada ya mama yake kuondoka siku kadhaa kwenda kuvuna maharage katika Kijiji cha Ikomela wilayani Mbozi.

Alisema alimfanyia ukatili huo huku akimtishia kumpiga ikiwa atasema kwa majirani au kwa mama yake mzazi atakaporudi nyumbani kutoka shambani.

Akizungumza nje ya mahakama baba mdogo wa mtoto aliyepewa mimba, Atupele Kamendu alisema baada ya kupata taarifa za mtoto wao kupewa ujauzito na baba yake mlezi walifanya jitihada za kumkamata alikokuwa akijificha wakishirikiana kwa ukaribu na shemeji yake ambaye ndiye mama yake mtoto aliyebakwa na kupewa ujauzito.