Wiki ya Uendelezaji wa Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) imeanza Jumapili mjini Harare, nchini Zimbabwe, kwa wito wa kuharakisha ukuaji wa viwanda katika kanda hiyo.
Wiki ya Uendelezaji wa Viwanda ya SADC ambayo inafanyika kwa mara ya saba, ni jukwaa kubwa zaidi la ushirikishwaji wa umma na binafsi lenye lengo la kuhimiza maendeleo ya viwanda na kukuza biashara na uwekezaji barani Afŕika.
Wiki hiyo imewakutanisha wadau wa sekta ya viwanda kutoka nchi 16 wanachama wa SADC, zikiwemo Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, na Zimbabwe.
Wiki ya viwanda ya SADC inatangulia Mkutano wa kawaida wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliopangwa kufanyika Agosti 17 nchini Zimbabwe.
Waziri wa Utangazaji, Habari na Huduma za Utangazaji wa Zimbabwe Bw. Jenfan Muswere, amesema wiki hii itaonesha fursa za uwekezaji katika minyororo mbalimbali ya thamani na kuwezesha mtandao miongoni mwa wadau katika sekta ya viwanda.