Kenya imewasilisha rasmi ombi la kiongozi mkongwe wa upinzani na waziri mkuu wa zamani Bw. Raila Odinga, kugombea uenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 2025.
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bw. Korir Sing'Oei amesema amewasilisha ombi la Bw. Odinga kwa kiongozi wa mabalozi wa Kanda ya Mashariki ambaye pia ni balozi wa Mauritius Bw. Dharmraj Busgeeth.
Nafasi ya mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika inatarajiwa kuwa wazi Februari 2025, kwani mwenyekiti wa sasa Bw. Moussa Faki kutoka Chad atamaliza muhula wake wa pili.
Bw. Faki aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017, na alishinda muhula wa pili mwaka 2021.