Rais Xi Jinping wa China ambaye pia ni katibu mkuu wa Kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China(CPC), ametaka juhudi zaidi kufanywa ili kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mwaka 2024.
Kamati kuu ya CPC imefanya mkutano uliohudhuriwa na watu wasio wanachama tarehe 26 mwezi Julai ili kusikiliza maoni na mapendekezo yao kuhusu hali ya sasa ya kiuchumi na kazi husika zitakazofanywa katika nusu ya pili ya mwaka huu. Rais Xi alipohutubia mkutano huo amesema kanuni ya kimsingi ya kuhimiza maendeleo huku kuhakikisha utulivu, inapaswa kuendelea kufuatwa kwenye kazi za kiuchumi katika nusu ya pili ya mwaka huu.
Ametaka juhudi kuimarishwa katika kutekeleza kikamilifu na kwa uaminifu falsafa mpya ya maendeleo katika pande zote, kuendeleza ujenzi wa muundo mpya wa maendeleo na kukuza nguvu mpya za uzalishaji kwa kuzingatia hali halisi na kuhimiza maendeleo yenye ubora wa juu. Pia amesisitiza kuimarisha mageuzi kwa kina, kuhimiza hamasa ya washiriki wa soko, kutuliza matarajio ya soko, kuongeza msukumo wa ufufukaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.