Kenya na Uganda zimeanza rasmi mazungumzo ya kupanua bomba la kusafirisha mafuta ya petroli kutoka Eldoret magharibi mwa Kenya hadi mjini Kampala.
Kampuni ya Kenya Pipeline (KPC) imesema mradi huo, unaoelekea kuathiri soko la mafuta kutoka nje ya eneo hilo, utahusisha ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Malaba kwenye mpaka wa Kenya na Uganda.
KPC pia imesema Uganda itakuwa na jukumu la kujenga njia ya kuunganisha bomba hilo hadi Kampala, wakati upanuzi wa baadaye utakuwa ni kuelekea mjini Kigali Rwanda.
Mkurugenzi Mkuu wa KPC Bw. Joe Sang amesema kwenye taarifa iliyotolewa mjini Nairobi, kuwa upanuzi wa bomba hilo hadi Uganda ni hatua ya kimkakati kwa Kenya wakati inatafuta kurejesha faida yake ya ushindani kwenye soko la nje la mafuta ya petroli, haswa kwa kuzingatia mkakati mpya wa Uganda wa uagizaji wa mafuta.