Angola yaandaa mkutano wa amani DRC
2024-07-31 22:52:21| cri

Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola Jumanne iliandaa mkutano wa pili wa mawaziri kuhusu usalama na amani ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) huko mjini Luanda, huku mawaziri wa mambo ya nje kutoka DRC na Rwanda wakihudhuria.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa wizara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Tete Antonio, alieleza imani yake kwamba pande hizo zitafikia makubaliano wakati wa mkutano huo, na kuandaa mapendekezo madhubuti yenye lengo la kurejesha amani na kunyamazisha bunduki mashariki mwa DRC.

Mkutano huo ulichukua takriban saa moja, hata hivyo, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu matokeo ya mkutano.

Mkutano huo wa Jumanne ulifuatia mkutano wa mawaziri uliofanyika Machi 21 mjini Luanda, ambapo wajumbe walikubaliana kuhusu umuhimu wa kupatikana kwa amani endelevu mashariki mwa DRC, pamoja na kukuza maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii. Makubaliano hayo yalihusisha kusitisha uhasama, kutekeleza usitishaji vita, na kuondoa majeshi.