Kenya imetangaza mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) baada ya virusi vya homa hiyo kugunduliwa kwa mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya katika kituo cha mpakani cha Taita Taveta, kusini mashariki mwa mji wa Nairobi.
Taarifa iliyotolewa na katibu Mkuu wa wizara ya afya ya Kenya, Bibi Mary Muthoni Muriuki amewashauri Wakenya kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga wao wenyewe, familia zao na jamii dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo. Amesisitiza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo katika Afrika Mashariki ikizingatia msongamano mkubwa wa watu kati ya Kenya na nchi nyingine za eneo hilo. Pia amesema wizara ya afya ya nchi hiyo imeahidi kudhibiti na kukinga maambukizi ya ugonjwa huo kadri iwezekanavyo ikishirikiana na serikali za kaunti, vituo vya afya forodhani na mashirika husika ya serikali.