Tanzania inawavutia wawekezaji wa China
2024-08-01 23:22:26| cri

Takriban wawakilishi 100 wa makampuni ya biashara na wawekezaji wa China wapo nchini Tanzania kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana nchini humo.

Maeneo makuu ya uwekezaji yanayolengwa na wawekezaji ni pamoja na sekta ya nishati, hususan katika vifaa vya nishati ya jua, sekta ya viwanda, sekta ya ujenzi, viwanda vya usindikaji wa chakula, na sekta ya madini.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji la China na Tanzania.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo Bw Teri alisema ziara ya hivi karibuni ya wawekezaji hao ni matokeo ya juhudi za serikali kuweka mazingira mazuri ambayo yamechochea ukuaji wa biashara na kuvutia uwekezaji nchini humo.

Kwa upande wake, Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, aliwahimiza Watanzania wengi zaidi kujitokeza na kutumia fursa hizo kwa kuanzisha ubia wa kimkakati wa kiuchumi na wawekezaji kutoka China. Alisema hii itawawezesha kupata mitaji na kupata ujuzi mpya wa kiteknolojia kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ujumbe na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikiano ya Tanzania na China, Bi. Betty Xu, alisema wawekezaji mbalimbali kutoka China wamekwenda Tanzania kujionea fursa mbalimbali zilizopo ili kuwekeza.