ATMIS yaimarisha mafunzo kuhusu ulinzi wa raia katika maeneo ya mapigano
2024-08-01 09:15:07| CRI

Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia ATMIS imesema, wafanyakazi 26 hivi wa tume hiyo wamemaliza mpango wa mafunzo ya siku tano kuhusu ulinzi wa raia.

Mafunzo hayo yanazingatia sheria ya kibinadamu ya kimataifa na sheria ya haki za binadamu, ambayo yanaendana na lengo la Tume ya Umoja wa Afrika kuunga mkono mkakati wa utulivu wa taifa wa Somalia ili kuhakikisha usalama wa taifa baada ya tume hiyo kuondoka.

Ofisa wa mradi katika Mfumo wa Utekelezaji na Uwajibikaji wa Umoja wa Afrika Bw. Ferdinand Nintunze, amesema, mafunzo hayo ni muhimu kwa wafanyakazi wa tume hiyo wakiwemo wanajeshi, askari polisi na raia, ambao kimsingi wanahusiana na kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Mradi huo wa mafunzo ni sehemu ya juhudi za tume ya ATMIS zinazoendelea kutoa kipaumbele kwa ulinzi wa raia, kwa mujibu wa azimio la 2628 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa (2022).