Serikali ya Zanzibar ya Tanzania imepongeza mradi wa msaada wa China katika kudhibiti ugonjwa wa kichocho, ikisema umesaidia kutokomeza ugonjwa huo katika visiwa hivyo.
Pongezi hizo za dhati zimetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Habiba Hassan Omar na Mratibu wa Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali wakati walipotembelea Mradi wa Msaada wa China wa Kudhibiti Ugonjwa wa Kichocho visiwani Zanzibar.
Dkt. Habiba aliishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono kwa dhati kazi ya afya ya Zanzibar kwa miaka mingi na pia kushukuru kikundi cha wataalamu wa kudhibiti ugonjwa wa kichocho kutoka China kwa juhudi zao za kutokomeza ugonjwa huo Zanzibar na kuwasaidia wananchi wa eneo hilo kuondokana na madhara yatokanayo na ugonjwa huo. Anatarajia kuwa taasisi ya Jiangsu ya magonjwa ya vimelea, kitengo mahususi cha kutekeleza mradi huo, itaongeza uhamishaji wa teknolojia, kutoa msaada zaidi katika mafunzo ya kujenga uwezo kwa wafanyakazi wa Zanzibar, kukuza vipaji bora vya kudhibiti ugonjwa wa kichocho, na kufikia lengo la kutokomeza kichocho haraka iwezekanavyo.