Rais wa Nigeria Bola Tinubu Jumapili alitoa wito wa kusitishwa kwa maandamano yanayogharimu maisha ya watu ambayo yanaendelea kote nchini, huku akiwataka raia wanaoandamana kutoa nafasi ya kufanya mazungumzo na serikali.
Akilihutubia taifa Jumapili asubuhi, Tinubu alielezea machungu ya watu kupoteza maisha na uharibifu wa majengo ya umma na binafsi wakati wa maandamano, akisema hali hiyo ni kinyume na ahadi iliyotolewa na waandaaji wa maandamano hayo yaliyoanza Alhamisi.
Hata hivyo kiongozi huyo wa Nigeria alikiri kuwepo kwa matatizo ya kiuchumi nchini humo, akieleza kuwa uchumi umeendelea kuwa na "mapungufu" kwa miongo kadhaa na kudorora kwa sababu ya "mielekeo mingi isiyo sahihi ambayo imedumaza ukuaji huo".
Hivyo ili kushughulikia matatizo ya wananchi, Tinubu aliapa kuendelea kufanya mageuzi yatakayokuwa na manufaa kwa Wanigeria wote, kuboresha na kupanua miundombinu ya kitaifa, na kutoa fursa zaidi kwa vijana.
Kiwango cha mfumuko wa bei nchini Nigeria kilipanda hadi asilimia 34.19 mwezi Juni na kupelekea gharama za maisha kuwa mbaya zaidi.