Kampuni za Tanzania na China zasaini mradi wa uchimbaji madini ya chuma wenye thamani ya dola milioni 77 za kimarekani
2024-08-05 09:23:37| CRI

Shirika la Taifa la Mendeleo (NDC) la Tanzania na kampuni ya Hexingwang ya Fujian, China wamesaini makubaliano, ili kuendeleza mradi wa uchimbaji wa chuma wa Maganga Matitu katika mkoa wa Njombe.

Kusainiwa kwa mradi huu wenye thamani ya dola milioni 77.4 unaotaka kuzalisha chuma cha sifongo kama malighafi kwa viwanda vya chuma kumeshuhudiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Bw. Doto Biteko jijini Dar es Salaam.

Akitoa hotuba fupi baada ya makubaliano kusainiwa, Bw. Biteko amesema mradi huo unatarajiwa kuhimiza ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo kupitia maendeleo ya viwanda.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya NDC Bw. Nicolaus Shombe amesema, mradi huo wa chuma uliopo katika eneo la kilomita za mraba 19.63, ni sehemu ya mradi wa chuma wa Liganga ulioko katika wilaya ya Ludewa.