Tume ya Misaada ya Kibinadamu ya Sudan (HAC) Jumapili ilikanusha madai ya kuwepo njaa huko Zamzam, moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi wa ndani katika Jimbo la Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan.
Katika taarifa yake tume hiyo ilisema kilichoelezwa katika ripoti ya Mtandao wa Mifumo ya Tahadhari ya Mapema ya Njaa (FEWS NET) hakina ukweli wowote.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa ripoti ya HAC katika Jimbo la Darfur Kaskazini ya Agosti 3 ilionesha kuwa ziara ya pamoja ya mashirika husika ya serikali na baadhi ya mashirika ya kimataifa kwenye kambi ya Zamzam iliyofanywa Julai 23 ilieleza hali ya utulivu wa kibinadamu huko.
Hivyo HAC imekanusha madai hayo na kusisitiza kuwa uhaba wa chakula na misaada ya kibinadamu katika maeneo na kambi hizi unatokana na kuzingirwa na waasi wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na mashambulizi ya mizinga yanayoendelea ya wanamgambo hao kwenye vituo vya afya na kambi.
Alhamisi iliyopita, FEWS NET, ilitoa tahadhari kwamba njaa inaendelea katika kambi ya Zamzam.