Mashirika ya kimataifa yatoa tahadhari ya ukame katika Pembe ya Afrika
2024-08-05 23:20:07| cri

Mashirika ya kimataifa yamesema Pembe ya Afrika itashuhudia uhaba wa mvua katika msimu wa mwezi Oktoba hadi Desemba, ambao unaweza kusababisha mazingira ya ukame.

Mashirika hayo ambayo ni Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ICPAC) kilicho chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), yamesema kuwa mifumo ya hali ya hewa imetabiri mabadiliko ya hali ya hewa ya La Nina katika nusu ya pili ya mwaka huu, ambayo inaweza kusababisha uhaba wa mvua.

Mashirika hayo yamewataka wenzi wa kibinadamu kushirikiana na serikali na nchi husika kuunga mkono mipango yao ya tahadhari, utekelezaji wa shughuli za maandalizi, na kutambua hatua husika za tahadhari ili kukabiliana na athari za uwezekano wa kuwa na mvua za chini kuliko kawaida.