Wizara ya Afya ya Tanzania Jumapili ilisema Tanzania imeimarisha usimamizi na udhibiti kwenye vituo vya kuingia nchini humo baada ya maambukizi ya mpox kuripotiwa katika nchi jirani za Burundi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Afya ya Tanzania Englibert Kayombo alisema, timu za wafanyakazi wa afya zimetumwa kwenye vituo vya mpakani nchini humo, ili kuimarisha usimamizi na udhibiti dhidi ya maradhi hayo. Alisema wafanyakazi wa afya wanafanya ukaguzi kwa wale wanaoingia na kutoka nchini humo. Hadi sasa, hakuna mtu yeyote wa Tanzania aliyethibitishwa kuambukizwa ugonjwa wa mpox.
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumatatu ilitoa wito kwa nchi zake nane wanachama kuwaelimisha wananchi wao jinsi ya kujilinda, ili kuzuia kuenea kwa mpox.