Watu wasiopungua 32 wamefariki dunia na wengine 107 kujeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha hivi karibuni na mafuriko yaliyokumba majimbo kadhaa ya Sudan.
Wizara ya Afya ya Sudan jana ilitangaza kuwa majimbo saba yaliathiriwa na mvua na mafuriko ambapo nyumba 5,575 ziliharibiwa. Mkurugenzi wa idara kuu ya dharura ya afya katika wizara hiyo Al-Fadil Mohamed Mahmoud alisema kuwa mvua kubwa na mafuriko yamesababisha matukio mengi ya kuharisha, ambapo watu 102 waliripotiwa katika jimbo la Kassala, wanne katika jimbo la Khartoum, na 16 katika jimbo la Gezira. Aliongeza kuwa hali ya afya katika majimbo mengine ilikuwa shwari, akibainisha kuwa wizara inachukua hatua muhimu za kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya msimu wa mvua.
Katika ripoti ya awali, Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Sudan ilitabiri kupanda kwa viwango vya maji katika Mto Gash, ambao unapita katika mji wa Kassala, mji mkuu wa jimbo la Kassala. Wananchi walitakiwa kuwa waangalifu na kukaa mbali na kingo za mto huo wa msimu.