Rais wa Kenya William Ruto Jumatatu alitia saini kuwa sheria Mswada wa Matumizi ya Ziada ya Fedha, unaopunguza matumizi ya serikali kwa shilingi bilioni 145.7 (kama dola bilioni 1.12 za Kimarekani).
Mswada huo mpya, ambao ulipitishwa na Bunge la Kitaifa Julai 31 baada ya rais kuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 kutokana na maandamano dhidi ya serikali, unalinda matumizi muhimu, pamoja na dola milioni 154 za kusaidia wakulima na kuongeza uzalishaji na tija.
Ili kusaidia mageuzi ya elimu, sheria mpya imetenga dola milioni 928.6, ikijumuisha kuajiriwa kwa walimu wa shule, na dola milioni 238.5 kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Pia imetenga dola milioni 124.6 kufadhili mageuzi ya sekta ya afya na kukuza Huduma ya Afya kwa Wote na dola milioni 27 kwa nyongeza ya mishahara kwa maafisa wa usalama wanaohudumu katika mashirika mbalimbali.
Juni 26, rais aliondoa Mswada tata wa Fedha wa 2024 ambao ulizua hasira ya umma kutokana na nyongeza nyingi za ushuru zilizochukiza watu.