Mamia ya Wasomali, wakiwemo maafisa wakuu wa serikali, wamefanya maandamano ya amani mjini Mogadishu, Somalia, ili kulaani kundi la itikadi kali la al-Shabab kufuatia shambulizi kali la hoteli lililosababisha vifo vya watu 37.
Wakikusanyika katika eneo la Lido Beach View ambapo shambulizi hilo lilitokea, waandamanaji walibeba mabango ya kuipinga al-Shabab na kulaani ukatili wa kundi hilo. Waliimba kauli mbiu za kuikemea na kuchukizwa na al-Shabab, pia walionyesha mshikamano wao kwa watu waliouawa na wengine 247 waliojeruhiwa katika shambulio hilo.
Miongoni mwa waandamanaji hao walikuwepo manusura, mawaziri na maafisa walioapa kutotishwa na ugaidi na kuwataka Wasomali kuungana na kushirikiana na vyombo vya usalama kukabiliana na ugaidi.