Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zitakazonufaika na mradi mkubwa wa ujenzi wa hospitali itakayokuwa na viwango vya kimataifa vya utoaji wa huduma za matibabu (AMCE).
Hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Umahili cha Kimatibabu cha Abuja, Nigeria, Bw. Brian Deaver, wakati Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mwigulu Nchemba alipotembelea ujenzi wa mradi wa hospitali ya aina hiyo nje ya mji wa Abuja.
Deaver amesema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 500 kwa wakati mmoja, na itatumia teknolojia ya kisasa kutibu magonjwa ya saratani ya damu na selimundu.
Pia amesema hospitali nyingine za aina hiyo zitajengwa katika nchi za Kenya, Ghana, na Tanzania, na zitatoa huduma za aina nyingi ikiwemo uchunguzi, matibabu, tiba kwa njia ya nyuklia na huduma nyingine.