Jeshi la Marekani laondoka kikamilifu nchini Niger
2024-08-06 22:53:06| cri

Awamu ya mwisho ya askari wa Jeshi la Marekani walioko Niger kama sehemu ya mapambano dhidi ya ugaidi ambao walianza kuondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Niamey, nchini humo Juni 7 mwaka huu, wamekamilisha zoezi hilo jana jumatatu katika mkoa wa Agadez, kaskazini mwa Niger.

Hafla ya kuashiria kufungwa kwa kambi ya ndege zisizo na rubani za jeshi la Marekani ilishuhudiwa na maofisa wa kijeshi wa Marekani na wa Niger.

Machi 16, serikali ya kijeshi ya Niger ilifuta makubaliano ya kijeshi yaliyoruhusu maafisa wa kijeshi na wafanyakazi ambao ni raia kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani kuwepo nchini humo, na Mei 19, majeshi ya nchi hizo mbili yalikubaliana kuhusu ratiba ya vikosi vya Marekani kuondoka Niger.