Hakuna shaka yoyote ile kwamba filamu ni sehemu ya dunia ya Sanaa, ikiwa ni njia inayotumia ubunifu mkubwa katika kuiwasilisha sanaa hiyo. Kwa miongo kadhaa sasa, tasnia ya filamu imekuwa ikitawaliwa na wanaume, mbele na nyuma ya kamera. Hata hivyo, miaka ya hivi karibuni yameshuhudiwa mabadiliko makubwa katika mandhari ya sinema, na ongezeko la uwepo wa wanawake wanaoongoza filamu. Pia ni muhimu kutambua vipaji na utofauti wa sauti za waongozaji wa kike kote duniani.
Mafanikio ya hivi karibuni kama vile filamu ya “Anatomy of a Fall” iliyoongozwa na Justine Triet mwanamke kutoka Ufaransa, yamethibitisha kuwa watengenezaji filamu wa kike wana mengi ya kutoa kama wenzao wa kiume. Ushindi huu, ingawa ni wa nadra, ni hatua muhimu kuelekea kutambuliwa kwa usawa zaidi na ubunifu kubwa wa wanawake. Wakati huo huo masuala ua usawa ambayo yanahimiza muundo wa washiriki wa filamu wenye uwakilishi sawa wa wanaume na wanawake, yameonesha matokeo chanya. Motisha hizi ni muhimu ili kukuza ushirikishwaji na utofauti ndani ya tasnia ya filamu. Hivyo katika kipindi cha ukumbi wa wanawake leo tutaangalia jinsi wanawake wanavyoendelea kufanya vizuri katika tasnia ya filamu.