Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Misri wafanya mazungumzo kuhusu hali ya Mashariki ya Kati
2024-08-07 09:00:36| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jana alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Misri Badr Abdelatty.

Wang alisema chini ya mwongozo wa kimkakati wa marais wa nchi hizo mbili, ushirikiano wa kimkakati wa kina kati ya China na Misri umepata maendeleo makubwa, na upo katika kipindi bora zaidi katika historia.

Pande hizo mbili pia zilibadilishana mawazo kuhusu hali ya Mashariki ya Kati. Wang alisema mauaji dhidi ya kiongozi mkuu wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran yamefanya hali ya eneo hilo kuwa hatari zaidi, na China inapinga na kulaani vikali vitendo hivyo vya mauaji vinavyokiuka misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, mamlaka na heshima ya Iran, na pia kudhoofisha sana juhudi za kukuza amani, na kufanya usitishaji mapigano huko Gaza kuzidi kushindwa kufikiwa. Amefahamisha kuwa China itaimarisha mshikamano na nchi za Kiarabu, na kufanya kazi na pande zote ili kuepusha kuongezeka na kuzorota zaidi kwa hali hiyo.

Kwa upande wake, waziri Abdelatty alisema kuwa Misri inathamini nafasi muhimu ya China katika kuhimiza amani Mashariki ya Kati, na kushukuru juhudi za China katika kuendeleza maridhiano ya ndani huko Palestina. Aliongeza kuwa Misri itadumisha ushirikiano wa karibu na China ili kuzuia kuongezeka zaidi kwa hali hiyo mbaya.