Waziri Mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi amesema mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika wa 2024, (FOCAC) uliopangwa kufanyika Septemba mjini Beijing, utaongeza uhai katika uhusiano wa pande mbili kati ya China na Kenya ambao umedumu kwa zaidi ya miongo sita.
Akiongea katika mkutano na wawakilishi kutoka jamii za Wachina huko Nairobi, Mudavadi, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje na diaspora alielezea matarajio ya nchi hiyo kwa mkutano huo ujao, katika uhusiano wake wa kidiplomasia na China. Amesema ushiriki wa Kenya katika FOCAC unathibitisha azma yao na uungaji mkono wao usioyumba kama mshirika wa kimkakati wa China kuandaa mkutano wenye mafanikio.
Wawakilishi wa Ubalozi wa China nchini Kenya, Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Jumuiya ya Wachina waishio Kenya, Chama cha Utalii cha Wachina nchini Kenya, Chama cha Wafanyabiashara wa China nchini Kenya, na makampuni ya biashara ya China nchini Kenya, walihudhuria mkutano huo kujadili maeneo ya kimkakati ya ushirikiano ili kuhimiza pande zote mbili kunufaika.
Balozi wa China nchini Kenya Zhou Pingjian alisema uhusiano wa nchi hizo mbili umeimarika kutokana na kuaminiana na matarajio ya pamoja.