Vifaa katika Bandari ya Sudan vyasubiri ruhusa ya kupelekwa kwenye kambi iliyokumbwa na njaa huko Darfur Kasakazini
2024-08-07 08:55:54| CRI

Afisa wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya kibinadamu alisema Jumanne kuwa vitu vya msaada vya kuokoa maisha tayari viko katika bandari kuu ya Sudan kwa ajili ya kupelekwa kwenye kambi ya Zamzam huko Darfur Kaskazini, ambako awali maafisa walitangaza kuwa kuna hali ya njaa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Operesheni na Utetezi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), Edem Wosornu alisema shehena hiyo ikiwa na vitu kama vile dawa muhimu, vifaa vya lishe, dawa za kusafisha maji na sabuni, vinasubiri idhini na uhakikisho wa usalama unaohitajika kabla ya kuweza kusafirishwa.

Wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya kibinadamu nchini Sudan, Wosornu aliwaambia wanachama kuwa ni muhimu ruhusa itolewe haraka kwa ajili ya kuhamisha vifaa kutoka Bandari ya Sudan hadi kwenye kambi iliyo karibu na mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, El Fasher.

Mkutano huo wa baraza uliitishwa siku chache baada ya Kamati ya Mapitio ya Njaa kuthibitisha kuwa hali ya njaa iko katika kambi ya Zamzam.