Rais wa Zambia atoa wito wa kufanyika makubaliano ya kimataifa kumaliza mzozo kati ya Russia na Ukraine
2024-08-07 08:58:39| CRI

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ametoa wito wa kuwepo kwa maelewano ya haraka ya kimataifa ili kumaliza mzozo kati ya Russia na Ukraine.

Amesema hayo alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Ivanovych Kuleba ambaye anatembelea nchini Zambia. Amesema kuwa mzozo wa Russia na Ukraine unahitaji kutatuliwa kwa njia za amani, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa ili kukuza utulivu na amani katika eneo hilo.

Aidha ametoa wito wa kuimarishwa kwa uhusiano wa pande mbili kati ya Zambia na Ukraine, hasa katika maeneo ya biashara na uwekezaji, kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine ameishukuru Zambia kwa mshikamano wake wa kisiasa na nchi yake, na kumpongeza Hichilema kwa kushiriki katika juhudi za kidiplomasia kumaliza mzozo huo. Ameongeza kuwa lengo la ziara yake ya Afrika ni kuendelea kujenga uhusiano na nchi za Afrika, akisisitiza haja ya kutafuta fursa mpya kati ya Zambia na Ukraine kwa kuimarisha ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pande zote mbili.