Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar Jumatano alitoa wito kwa balozi za nchi za nje kuepuka kuingilia maandamano yanayoendelea nchini humo ya kupinga gharama za maisha, akisema serikali inafanya kazi kwa bidii kushughulikia maswala ya raia.
Tuggar alitoa wito huo wakati akizungumza katika mkutano na wajumbe wa mabalozi mjini Abuja, akiitaka jumuiya ya kimataifa kutoa usaidizi wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kuhakikisha maisha bora kwa Wanigeria ndani na nje ya nchi.
Amesema wakati serikali inaendelea kujitahidi kufanya mageuzi mbalimbali ili kutatua changamoto zinazoikabili Nigeria na Wanigeria, ni kawaida kwamba hakuna taifa linalovumilia kuingiliwa na mataifa ya kigeni katika masuala yake ya ndani, akisisitiza kuwa nchi hiyo inaongozwa na utawala wa sheria na serikali itafanya kila iwezalo kulinda raia wake.
Ameonya kuwa serikali itachukua hatua zinazofaa dhidi ya taasisi yoyote ya kigeni iliyopo Nigeria, ambayo itagundulika kuwa imewaunga mkono moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja waandamanaji kwa njia zozote au kutaka kuingilia masuala ya ndani.