Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Jumatano ilisaini makubaliano na makampuni mawili yanayofadhiliwa na China ili kuimarisha maendeleo ya sekta ya afya na nishati nchini humo.
Kampuni ya dawa ya China, Africa Bio Chem, ilisaini makubaliano ya kujenga kituo cha kuzalisha dawa na chanjo. Kampuni nyingine ya China inayojishughulisha na uzalishaji wa umeme wa photovoltaic ya ABC Power Tech Ltd, pia inashirikiana na serikali ya Zanzibar kuzalisha megawati 200 za umeme katika eneo la viwanda.
Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi alishuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo ya uwekezaji, akisema makampuni hayo mawili ya China yatakuwepo katika eneo jipya la viwanda la Zuze lililopo Dunga.
Rais Mwinyi aliishukuru China kwa kupeleka dawa nyingi, kutoa mafunzo kwa watu wake na kuwajengea uwezo wananchi, akisema wanatarajia kuendeleza ushirikiano huu.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo, mshauri mkuu wa wanasayansi wa kampuni ya Africa Bio Chem, Yang Chen, alisema kampuni yake imeamua kuungana na Zanzibar kujenga kituo hicho ili kuchangia nguvu zake katika kuboresha kiwango cha afya katika visiwa hivyo na kanda nzima ya Afrika.