Wimbi jipya la maandamano lazuka tena nchini Kenya
2024-08-09 09:05:32| CRI

Maandamano ya kupinga serikali yamerejea tena barabarani nchini Kenya siku ya Alhamisi, na kusababisha majeruhi na zaidi ya watu 170 kukamatwa.

Maandamano hayo, ingawa yalikuwa madogo kuliko yale ya awali, yalifanywa na waandamanaji vijana ambao waliingia barabarani katika kaunti sita kati ya 47 za Kenya, wakiimba nyimbo za kuipinga serikali na kuonesha mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Katika mji wa Nairobi, biashara za kawaida zilikatizwa katika wilaya kuu ya biashara ambapo maduka yalifungwa na wafanyakazi wa ofisi wakikwepa eneo hilo. Usafiri wa umma ulisitishwa huku wahudumu wa matatu, wakiondoa magari yao kwa sababu za kiusalama. Maafisa wa usalama walipambana na waandamanaji wakitumia mabomu ya machozi na risasi za moto ili kuwatawanya. Waandamanaji walisema wanaipigania Kenya iliyo bora, na kutaka masuala yao kushughulikiwa, likiwemo kuongezeka kwa ukosefu wa ajira kwa vijana.

Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli aliwaonya waandamanaji dhidi ya vitendo visivyo halali, akisema kila Mkenya, ana uhuru wa kuandamana kwa mujibu wa sheria. Amewahakikishia kuwa serikali inashughulikia malalamiko ya maandamano yaliyopita na kuonya kuwa wahalifu watachukuliwa hatua kali.