Waziri Mkuu wa Libya Abdul-Hamid Dbeibah amesema serikali yake itasimama kithabiti dhidi ya mtu yoyote anayejaribu kuanzisha tena ukiukaji wa kijeshi na kuchochea utengano nchini humo.
Dbeibah amesema hayo wakati wa hafla ya kuhitimu kwa wanafunzi wa vyuo vya kijeshi iliyofanyika katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Amesisitiza kuwa wanaendelea kujenga jeshi lenye nguvu kwa imani ambayo msingi wake ni Mungu na taifa, na sio mtu binafsi wala kundi lolote.
Waziri Mkuu huyo amewataka wanafunzi waliohitimu kufuata nyayo za waanzilishi wa jeshi ili kuzuia matakwa ya nje na ndani ambayo yanataka kuirejesha nchi kwenye utawala wa kidikteta.
Libya imekuwa kwenye mvutano wa kisiasa tangu kuangushwa kwa utawala wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011, ikiwa na serikali mbili zinazopingana na nguvu kubwa za kigeni zikiingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.