Polisi nchini Kenya wawasaka wapiganaji wa al-Shabab baada ya shambulio mpakani mwa nchi hiyo
2024-08-12 08:39:53| CRI

Vikosi vya usalama nchini Kenya vimeanza kuwasaka wapiganaji wa kundi la al-Shabab waliomuua ofisa wa serikali kabla ya kuiba gari lake na kutoroka nalo katika Kaunti ya Mandera jumamosi iliyopita.

Kamishna wa Kaunti hiyo Henry Ochako amethibitisha tukio hilo jumapili na kusema, wapiganaji hao walifanya shambulio la ghafla dhidi ya ofisa huyo saa tisa alasiri kwa saa za huko katika eneo la Kamor mjini Mandera.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni wiki moja baada ya vikosi vya usalama kufanya operesheni katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya ili kuwaondoa wapiganaji wa kundi la al-Shabab katika eneo hilo.

Tangu jeshi la Kenya kuingia nchini Somalia mwaka 2011, mashambulio kadhaa yanayoaminika kutekelezwa na wapiganaji wa kundi la al-Shabab yametokea katika kaunti za Mandera, Wajir na Garissa zilizoko kaskazini mashariki mwa Kenya.