Ripoti yaonesha kuongezeka kwa ukatili wa kingono mtandaoni na unyanyasaji wa watoto
2024-08-12 11:00:20| cri

Ripoti mpya kutoka Mfuko wa Watoto wa Kimataifa Kanda ya Afrika na Jukwaa la Sera ya Mtoto la Afrika (ACPF) imeonesha kuwa watoto wenye umri wa kati ya miaka 12-17 nchini Kenya wanakabiliwa na ongezeko la kutisha la ukatili na unyanyasaji wa kingono mtandaoni.

Ripoti hiyo inafichua kuwa hadi asilimia 13 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 waliohojiwa wametishwa au kudanganywa ili kushiriki ngono mtandaoni. Hii inasisitiza kwamba vitendo kama hivyo vya unyanyasaji vinazidi kuenea, kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa teknolojia na mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa ACPF Dkt Joan Nyanyuki amesema mtazamo ulioenea kwamba uhalifu wa mtandaoni sio uhalifu wa kweli umezua mazingira ya ukiukaji wa sheria, ambapo Afrika inashuhudia tatizo ambalo linaongezeka kwa kasi, na ushahidi unaonyesha kuwa Afrika inaweza kuwa eneo jipya kwa wanyanyasaji wa ngono mtandaoni.

Zaidi ya hayo, ripoti inaonesha mwelekeo unaosumbua ambapo waathiriwa wengi wa ukatili na unyanyasaji wa kingono mtandaoni ni vijana wadogo sana.