Maporomoko ya ardhi kwenye dampo la taka nchini Uganda yasababisha vifo vya watu 21
2024-08-13 10:23:12| cri

Karibu watu 21 wamekufa baada kwenye ajali ya kuporomoka kwa udongo iliyotokea kwenye dampo kubwa la taka la Kiteezi mjini Kampala Uganda. Polisi wamesema waokoaji wanaendelea kuchimba taka kwa matumaini ya kupata wahanga baada ya ajali hiyo kutokea kufuatia mvua zilizonyesha kwa wiki kadhaa.

Dampo la Kiteezi lenye ukubwa wa ekari 36 ndio dampo pekee linalohudumia wakazi wote milioni nne wa mji wa Kampala. Meya wa Kampala Bw. Erias Lukwago amesema kuna uwezekano kuwa watu wengi zaidi wamefunikwa chini na kutaja ajali hiyo kuwa ni janga.

Rais Yoweri Museveni ameamuru kufanyika kwa uchunguzi kuhusu jinsi watu walivyoruhusiwa kuishi karibu sana na eneo hilo, na kuamuru watu walio kwenye hatari kuondolewa. Jumatatu asubuhi msemaji wa jeshi la polisi alisema miili 21 ilikuwa imepatikana, minne kati yao ilikuwa ni ya watoto, na msemaji wa polisi wa Kampala, Patrick Onyango amesema watu 14 wameokolewa.