Umoja wa Mataifa wasema watu 39 wauawa nchini Somalia katika mapigano ya silaha ndani ya miezi miwili
2024-08-13 08:46:36| CRI

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, watu 39 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea katika miezi miwili iliyopita nchini Somalia.

Katika ripoti yake ya hali ya kibinadamu iliyotolewa jana mjini Mogadishu, OCHA imesema mapigano hayo yalisababishwa na mgogoro wa ardhi, ambapo watu 35 waliuawa katika mkoa wa Mudug, katikati ya Somalia, na watu wengine wanne waliuawa katika mkoa wa Luuq, kusini mwa Somalia.

OCHA pia imesema, watu 42,000, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee walikimbia makazi yao kutokana na vurugu katika mkoa wa Luuq mwezi Julai, wakiwemo watu 12,000 waliokimbilia katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Ripoti hiyo imesema, familia karibu 96,000 zimeathiriwa na mapigano ya hivi karibuni ya kutumia silaha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi katika mkoa wa Galmudug nchini Somalia.