Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza mjini Harare, Zimbabwe jana jumanne, huku maofisa wakirejea tena ahadi yao ya kudumisha amani na usalama ili kuchochea maendeleo na maingiliano ya kikanda.
Akihutubia wakati akichukua nafasi ya uenyekiti wa zamu wa Baraza hilo, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Zimbabwe Frederick Shava amesema, SADC inapaswa kuendelea utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa kikanda ambao msingi wake ni amani, usalama na utawala bora. Amesema amani na utulivu ni mambo muhimu katika ajenda ya mageuzi ya kikanda, na bila ya hivyo, malengo na matarajio hayataweza kutimizwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa SADC Elias Magosi amesema Jumuiya hiyo inaendelea kujikita katika maingiliano ya kiuchumi na kijamii na kudumisha amani na usalama katika kanda hiyo.