Watunga sera, wanasyanasi na wamiliki wa viwanda kutoka China, Afrika, na Kituo cha Kimataifa cha Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) wamekutana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, na kuzindua jukwaa linalolenga kuendeleza mageuzi ya kilimo, kutimiza usalama wa chakula, na kukabiliana na umasikini katika maeneo ya vijijini barani Afrika.
Jukwaa la Kisayansi la Kituo cha Kimataifa cha Uboreshaji wa Mahindi na Ngano la China na Afrika, lililoandaliwa na Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China (CAAS) pamoja na Kituo hicho, limejikita katika Kubadili Mifumo ya Kilimo barani Afrika kupitia Uvumbuzi wa Kisayansi na Uhusiano.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho Bram Govaerts amesisitiza umuhimu wa jukwaa hilo, akisema linatoa fursa muhimu kwa wanasayansi wa China na Afrika kutafiti mikakati mipya ya kubadili mifumo ya chakula wakati wa changamoto kama mabadiliko ya tabianchi, wadudu wa mimea na magonjwa.
Makamu rais wa CAAS Ye Yujiang amesema, uhusiano wa kunufaishana kati ya wanasayansi wa China na Afrika unaweza kuchochea mageuzi ya kilimo, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kuboresha kipato cha vijijini.