Wasomi barani Afrika wamesema lengo la Afrika kutimiza mageuzi ya kijani linaweza kutimia haraka mara nchi za bara hizo zitakapoanza kutumia teknolojia mpya za kilimo, uvumbuzi, kutoa fedha za kutosha na kuboresha maingiliano ya soko.
Hayo yamesemwa katika Jukwaa la Kisayansi la Kituo cha Kimataifa cha Uboreshaji wa Mahindi na Ngano la China na Afrika, lililoandaliwa na Akademia ya Sayansi ya Kilimo ya China (CAAS) na Kituo cha Kimataifa cha Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT) linalofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 16 mwezi huu jijini Nairobi, Kenya.
Profesa Blessings Chinsinga wa Elimu ya Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Malawi amesema, bara la Afrika linatakiwa kuanzisha masoko yanayofaa, kuboresha matumizi ya teknolojia zinazofaa kwa wakulima wadogowadogo, na kurahisisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kama mbegu bora ili kuongeza mavuno.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Kiuchumi katika Idara ya Utafiti na Huduma za Kitaalamu nchini Zimbabwe, Tariro Gwandu amesisitiza kuwa, Afrika inapaswa kutumia nguvukazi ya vijana na majukwaa ya kidijitali, kufufua upya miundombinu ya umwagiliaji, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kutimiza mapinduzi ya kijani.